VIINGILIO Simba vs Bravos do Maquis 27 November 2024
VIINGILIO Simba vs Bravos do Maquis 27 November 2024
Klabu ya Simba SC itacheza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya Makundi ya CAF Confederation Cup 2024/2025 dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola November 27,2024.
Kuelekea mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo ametaja Viingilio ambapo Kwa Mzunguko itakuwa Tsh 5,000 tu.
Viingilio vingine ni Tsh 10,000 Kwa Viti vya rangi ya Machungwa, Tsh 15,000 Kwa VIP C, Tsh 20,000 Kwa VIP B na Tsh 50,000 Kwa VIP A, huku Platinum ambayo inajumuisha usafiri wa pamoja wakiwa na escort, eneo maalumu kukaa na chakula itakuwa Tsh 150,000 na Tanzanite ambayo ni VVIP, Gate Pass na jezi mpya itakuwa Tsh. 250,000.

Viingilio vya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Bravos. #WenyeNchi #NguvuMoja
Aidha Ahmed Ally ameitaja tarehe 24 kuwa ndiyo siku ya rasmi ya uzinduzi wa hamasa Kuelekea mchezo huo wa kwanza wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup 2024/2025).
“Tarehe 24 ndio utakuwa uzinduzi rasmi wa hamasa, hekaheka zitaanza siku hiyo. Tutaanzia kwenye tawi la Simba Bomba Mbili kwa Chela lipo Mombasa Midizini. Tutafanya balaa kubwa kuanzia saa 5 asubuhi. Tukimaliza hapo tutakwenda uzinduzi part two Kiwalani Minazi Mirefu. Siku hiyo toka nyumbani umejiandaa.”
“Tarehe 25 siku ya Jumatatu itakuwa siku ya kuchangia damu, mmemsikia Mwenyekiti Mangungu amelisema hilo. Tutawatangazia vituo vya Mbagala, Karume kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania wenzetu. Na inaweza kukusaidia wewe mwenyewe au ndugu yako.”
“Tarehe 26 tutakuwa na tour kuanzia Temeke, Mtoni kwa Aziz Ally kwenda hadi Mbagala kuwambia Wanasimba umuhimu wa mchezo huo na kuwauzia tiketi.”
“Tarehe 27 itakuwa siku ya mchezo na uchaguzi wa serikali za mtaa lakini pia siku hiyo itakuwa siku ya mapumziko. Mwanasimba asubuhi utapiga kura na baada ya hapo moja kwa moja safari Uwanja wa Mkapa kwenda kuishangilia timu yako ya Simba Sports Club.”
“Mchezo huo ni wa kwanza wa makundi na lazima tuanze vizuri kwa kupata ushindi na ili kupata ushindi lazima kufanya kazi kubwa. Siku hiyo lazima tukaujaze uwanja, mkiujaza uwanja tutakuwa katika sehemu nzuri ya kupata ushindi. Tutumie nguvu zetu zote kuhakikisha tunapata ushindi.”
“Tunataka mechi zetu ndio ziwe zenye mvuto zaidi kuliko mechi zote kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Kama unajijua hujawahi kwenda Uwanja wa Mkapa hii ndio mechi yako.”
“Mara ya mwisho Kombe la Shirikisho Afrika tulitolewa na Orlando Pirates pale Afrika Kusini, mwaka huu breaki ya kwanza ni nusu fainali na pale na fainali ni karibu sana. Na timu ya kutufikisha hapo TUNAYO.” alimaliza Ahmed Ally
