VIGEZO na Sifa za Kujiunga na Jeshi la Polisi
VIGEZO na Sifa za Kujiunga na Jeshi la Polisi, Jeshi la Polisi Tanzania ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kudumisha amani, Usalama, na Utulivu Nchini.
Ili kutimiza wajibu huu mkubwa, Jeshi la Polisi huhitaji kuajiri vijana wenye Sifa, Ari, na Uzalendo wa hali ya juu watakao fanikisha nia na malengo ya Jeshi.
Jeshi la polisi limefungua mfumo wa kupokea maombi mapya ya ajira kwa vijana wa Kitanzania wenye ndoto ya kutumikia nchi yao kupitia Jeshi la Polisi.
Kupitia Makala hii utapata mwanga wa kutosha kuhusu Vigezo na Sifa za Kielimu, Maumbile na Nyenginezo maalum, mchakato wa kuomba, na vidokezo vya kukusaidia katika safari yako ya kuwa Askari Polisi nchini Tanzania.
Ili kujiunga na Jeshi la Polisi Tanzania mwombaji anatakiwa kutimiza sifa zifuatazo:
- Mwombaji awe raia wa Tanzania kwa kuzaliwa, mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 25 kwa waombaji wa kidato cha nne, sita, na astashahada.
- Au kati ya miaka 18 na 30 kwa waombaji wa shahada na stashahada.
- Waombaji wa kidato cha nne wawe wamehitimu kuanzia mwaka 2018 hadi 2023 na wawe na daraja la I hadi IV, wenye daraja la IV wawe na alama 26 hadi 28.
- Waombaji wa kidato cha sita wawe wamehitimu kuanzia mwaka 2018 hadi 2023 na wawe na daraja la I hadi III.
- Waombaji wa astashahada, stashahada, na shahada wawe wamehitimu katika fani zinazohitajika na Jeshi la Polisi.
- Wanaume wawe na urefu usiopungua futi 5 na inchi 8, wanawake wawe na urefu usiopungua futi 5 na inchi 4.
- Mwombaji awe na kitambulisho cha taifa au namba ya utambulisho kutoka NIDA.
- Awe na uwezo wa kuwasiliana kwa ufasaha katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
- Pia, anatakiwa kuwa na afya njema ya kimwili na kiakili, iliyothibitishwa na daktari wa serikali.
- Aidha, mwombaji anatakiwa awe hajaoa/kuolewa na hana mtoto.
- Ni sharti pia kwamba hajawahi kutumia dawa za kulevya na yuko tayari kuhudhuria mafunzo ya awali ya taaluma ya polisi.
- Mwombaji hapaswi kuwa ameajiriwa na taasisi yoyote ya serikali.
- Zaidi ya hayo, anatakiwa kuwa tayari kufanya kazi za polisi popote nchini Tanzania, kujigharamia katika hatua zote za usaili, asiwe na alama za kuchorwa mwilini, na asiwe na kumbukumbu za uhalifu.
