Ugonjwa wa Bawasiri, dalili na tiba yake
Ugonjwa wa Bawasiri, dalili na tiba yake
Bawasiri ni nini?
Bawasiri ni kuvimba kwa mishipa ya damu iliyopo ndani ya au katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa.
Ni hali ambayo inaweza kusababisha nyama kujitokeza nje, hivyo bawasiri inaweza kuwa bawasiri ya ndani au bawasiri ya nje.
Kuna aina kuu mbili za bawasiri ambazo ni;
- Bawasiri ya nje
- Bawasiri ya ndani.
Bawasiri hii ya ndani ndio bawasiri mbaya kabisa kwa sababu ni vigumu mgonjwa kujitambua kua anatatizo na hii inatokana na tabia ya bawasiri ya ndani kutokua na maumivu wakati inaanza.
Ugonjwa huu unaweza kusababisha mwasho, maumivu na damu au kamasi kutoka wakati wa kujisaidia haja kubwa ingawa wakati mwingine hauna dalili.
Madhara ya bawasiri ya ndani ni pamoja na damu kutoka wakati wa kujisaidia, damu kuganda ndani ya mishipa ya damu na maumivu.
Ugonjwa huu umekua ni ugonjwa hatari kutokana na tabia za wagonjwa kuficha kutokana na aibu ya tatizo lenyewe lilipo au kuhofia jamii kumtazama tofauti kwa sababu jamii nyingi hasa za afrika mashariki zinaamini kuwa ugonjwa huu ni mkosi mkubwa.
Kutokea kwa bawasiri kunaweza kuhusishwa na hali kama uzee, ujauzito, kuharisha au choo kufunga (constipation), saratani kwenye nyonga au kuketi kwa muda mrefu.
Tiba ya bawasiri inategemea aina ya bawasiri na ukubwa wa tatizo, Matibabu ya bawasiri yanaweza kuhusisha matumizi ya dawa au upasuaji mdogo.
Dalili za Bawasiri
Inakadiriwa 40% ya watu wenye bawasiri hawana dalili za moja kwa moja, dalili za bawasiri hujumuisha maumivu, mwasho na hisia ya kitu kinachokera katika eneo linalozunguka njia ya haja kubwa.
Baadhi ya watu hupata shida kujisaidia haja kubwa na hutokwa damu wanapojisaidia, wakati mwingine mishipa ya damu huweza kujitokeza nje.
Ikiwa hali hii inatokea, inawezekana kuhisi uvimbe mdogo katika eneo husika.
Vihatarishi vya Bawasiri
Bawasiri hutokea pale shinikizo huongezeka kwenye mishipa ya damu inayozunguka njia ya haja kubwa.
Hii huweza kuwa matokeo ya kitu kinachokandamiza utumbo, kama vile wakati wa ujauzito, au huweza kutokea kutokana na kujikamua sana wakati wa haja kubwa kutokana na kufunga choo au kuharisha kwa muda mrefu.
Hali hii hutokea sana na hutokea zaidi kadri umri unavyoongezeka, watu wenye uzito wa kupita kiasi wana uwezekano mkubwa wa kupata bawasiri.
Vitu vingine vinavyoongeza hatari ya kupata bawasiri ni pamoja na;
- Kuwa na uzito wa mwili kupita kiasi, ujauzito, na kula vyakula visivyo na nyuzinyuzi (fibre) za kutosha.
- Kubeba vitu vizito mara kwa mara.
- Kuhara kwa muda mrefu na kufunga choo (constipation)
- Kujamiiana kinyume na maumbile.
- Historia ya uwepo wa ugonjwa wa bawasiri katika familia.
- Magonjwa yanayoathiri njia ya haja kubwa
- Kuketi kwa muda mrefu (Madereva)
- Uzee na matatizo ya kutopata choo pamoja na
- Kuwa na mgandamizo mkubwa tumboni.
Utambuzi wa Bawasiri
Utambuzi hufanywa na daktari kwa kuchukua maelezo ya mgonjwa na kuchunguza njia ya haja kubwa.
Uchunguzi wa njia ya haja kubwa hujumuisha kuangalia eneo hili na kuingiza kidole taratibu kuchunguza sehemu ya ndani ya njia ya haja kubwa.
Ikiwa bawasiri hazionekani kirahisi, au sababu ya kutoka damu haijaeleweka vizuri, uchunguzi wa ziada huweza kufanywa ili kuhakikisha hamna sababu nyingine ya dalili hizi.
Athari za Bawasiri
- Upungufu wa damu mwilini
- Kutokwa na kinyesi bila kijitambua
kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa - Kupungukia nguvu za kiume (kwa wanaume)
- Kupungukiwa na uwezo wa kufanya kazi kutokana na maumivu na
- Kupata tatizo la kisaikolojia
Namna ya Kujikinga dhidi YA Bawasiri
- Kula mboga za majani na nafaka zisizo kobolewa kwa wingi
- Kunywa maji mengi lita sita hadi kumi na mbili kwa siku
- Acha kufanya ngono kwa kutumia tundu la haja kubwa (kulawitiwa)
- Punguza kukaa chooni kwa muda mrefu, kunaweza kuongeza
- shinikizo katika njia ya haja kubwa.
Aina za Bawasiri
Bawasiri ya ndani: hii hutokea ndani ya mfereji wa haja kubwa na huwa haiambatani na maumivu na wengi huwa hawajitambui kuwa wana tatizo hili
Aina hii hutokana na kuvimba na kuharibika kwa mshipa wa artery za ndani ya mfereji wa haja kubwa
Aina hii ya bawasiri imegawanyika katika madaraja manne kama ifuatavyo;
- Daraja la kwanza: hii ni bawasiri ambayo haitoki mahali pake pa kawaida.
- Daraja la pili: hii hutokea wakati wa haja kubwa na kurudi yenyewe baada ya kujisaidia
- Daraja la tatu: hii hutokea wakati wa haja kubwa na mtu kuweza kurudisha ndani yeye mwenywe.
- Daraja la nne: hii ni bawasiri inayotoka na huwa ngumu kurudi
Bawasiri ya nnje
Aina hii ya bawasiri hutokea katika eneo la mwisho kabisa la mfereji wa haja kubwa na huambatana na maumivu makali na kuwashwa kwa ngozi katika eneo la tundu hilo pia husababisha mishipa ya damu (VENA) kupasuka na damu kuganda na kasababisha Aina ya bawasiri iitwayo thrombosed hemorrhoids
Matibabu ya Bawasiri
Bawasiri inatibika na kuna njia mbalimbali za kutibu bawasiri.
Tiba halisi ya bawasiri ni kuhakikisha kupata choo kilaini na kuepuka kufunga choo, ili kuepuka hali kuwa mbaya zaidi.
Krimu za kupaka na dawa za kuingiza katika njia ya haja kubwa (suppositories) zinaweza kusaidia kupunguza uvimbe, mwasho na maumivu, dawa hizi hupatikana katika maduka ya dawa.
Kuna matibabu mengine ambapo sindano au kamba maalum hutumika ili kupunguza ukubwa wa mishipa ya damu.
Aidha dawa ya bawasiri sugu ni kufanya upasuaji.
