SIMBA yawaita Mashabiki CCM Kirumba
SIMBA yawaita Mashabiki CCM Kirumba
Klabu ya Simba SC inatarajiwa kucheza mchezo unaofuata wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Pamba Jiji FC Ijumaa ya Novemba 22,2024 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Kuelekea mchezo huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally amewataka wakazi wa Mwanza na maeneo ya jirani kujiandaa kwa mchezo huo ambao hakuna matokeo mengine wanayohitaji zaidi ya ushindi.
Ahmed amesema kuwa Ligi ya Msimu huu ni kama vita, wanapaswa kushinda kila mechi inayokuja mbele yao kwani kama hawatafanya hivyo watawapa faida wengine.
“Kikosi kwa sasa kinaendelea na programu ya mazoezi kikijiandaa na mchezo dhidi ya Pamba. Leo usiku tutaondoka kwenda Mwanza na wachezaji wanne waliokuwa Taifa Stars na Camara aliyekuwa timu ya taifa ya Guinea wameshajiunga na kambi. Steven Mukwala atawasili Dar kesho alfajiri na kuunganisha kwenda Mwanza”
“Kesho tukiwa Mwanza tutatembelea Kituo cha Kutunza Watoto Yatima cha Ilemela kurudisha kwa jamii. Wanahabari tutaondokea benki ya NBC kesho saa 4 asubuhi baada ya mkutano wa wanahabari ambao kocha na mchezaji watazungumza.”
“Mchezo dhidi ya Pamba ni muhimu mno kushinda sababu utatupa ujasiri kuelekea mchezo dhidi ya Bravos. Nichukue nafasi hii kuwambia mashabiki wetu wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwamba waangalie Pamba kama mpinzani wetu mgumu kwa maana hiyo wafanye maandalizi makubwa ya kwenda kumuangamiza Pamba. Tunahitaji ushindi huo.”
“Hakuna uzalendo kwa watu wa Mwanza kwenye mchezo huo, tusiposishinda itakuwa faida kwa watu wengine. Tusimame kwanza na Simba na uzalendo utarudi baada ya kushinda. Hata uwe nani simama na Simba yako, hii vita sio ya Pamba wao wametumwa tu,” alisema Ahmed
