SIMBA Yasaini Mkataba Kampuni ya KNAUF
SIMBA Yasaini Mkataba Kampuni ya KNAUF
Klabu ya Simba SC imeingia mkataba wa mwaka mmoja na Kampuni ya kuzalisha bidhaa za ujenzi ya KNAUF kutoka nchini Ujerumani.
KNAUF ni wanazalisha bidhaa zenye hadhi ya Ujerumani nchini Tanzania, ambazo ni Jipsam bodi, Jipsam plasta na nyinginezo nyingi.
Mkurugenzi wa Kanda Afrika Mashariki ya KNAUF, Ilse Boshoff amesema kuwa uhusiano huu ni mkubwa ambao utakuwa na faida kwa pande zote mbili kitaifa na Kimataifa na ndicho kilivyowavutia kuja Simba.
Bi Boshoff amesema kuwa KNAUF inatengeneza bidhaa bora za ujenzi na ilianza kufanya kazi nchini Tanzania tangu mwaka 2015 na tayari imewekeza kiasi cha bilioni 148.
“Tupo nchi zaidi ya 90 duniani na malengo yetu ni kuzidi kujitanua zaidi na matumaini yetu uhusiano huu na Simba utakuwa msaada kwetu kuendelea kujulikana zaidi tukiendelea kuzalisha bidhaa bora za ujenzi kutoka Ujerumani,” amesema Boshoff.
Naye Mwenyekiti wa Klabu, Murtaza Mangungu amesema kuwa mkataba huu utakuza chapa ya KNAUF pamoja na Simba pia, ambapo amesema hatukuangalia thamani yake bali umuhimu wa kuendelea kujitangaza kimataifa.
“Sisi kama Simba hatukuangalia zaidi thamani ya mkataba bali tumeangalia kujitangaza na kuyavutia makampuni mengine ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza kwetu na tunawakaribisha,” amesema Mangungu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu, Ahmed Ally naye amewaomba Wanasimba kununua bidhaa kutoka kwa KNAUF kwakuwa wamejiridhisha kuwa vifaa vyao ni bora na vinaendana na klabu ya Simba.
“Mwanasimba yoyote anayetaka kujenga hasa akiwa kwenye hatua ya kumalizia ujenzi wake, Kampuni ya Knauf imekuja kwa ajili yake. Sisi tumejiridhisha kuwa Knauf inazalisha bidhaa bora kabla ya kukubali mkataba huu kwahiyo Wanasimba wote tunatakiwa kuiunga mkono,” amesema Ahmed.
