RAIS Dkt. Samia Aongeza Muda wa Uokoaji Kariakoo
RAIS Dkt. Samia Aongeza Muda wa Uokoaji Kariakoo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza kwa njia ya simu akiwa Brazil kuhusiana na zoezi la uokoaji katika jengo lililoporomoka eneo la Kariakoo amemuelekeza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuongeza saa 24 za uokoaji.
“Mhe. Waziri Mkuu, ninatambua utaratibu wa uokoaji una muda maalum wa saa 72 mpaka kusitisha zoezi hilo. Binafsi nina matumaini kuwa Mwenyezi Mungu anaweza akatenda miujiza yake na kuweza kuwanusuru ndugu zetu wengine ambao bado wamenasa kwenye jengo hilo. Ninakupa maelekezo ya kutositisha zoezi la uokoaji na kuongeza muda wa saa 24 zaidi ili kuwapambania ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai” amesema Rais Samia kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa B. Nyanga
“Kwa vikosi vyetu vyote na wananchi wote wanaopambana kuokoa maisha ya ndugu zetu katika zoezi hilo ninaomba ufikishe salamu zangu na uwaeleze kuwa natambua na nina wathamini sana. Wameonyesha utu, uzalendo mkubwa na uchapakazi wa hali ya juu sana. Hivyo nawatia moyo na kuwapa nguvu ya kuendelea kuwapambania ndugu zetu kwani ninyi ni mashujaa wa taifa letu”
Kwa upande mwingine, Rais Dkt. Samia amewasihi wananchi, ndugu na jamaa kuendelea kuwa na subira na kama taifa tuendelee kuwaombea ndugu zetu na wapiganaji wetu ili tufanikishe zoezi hili kwa mafanikio makubwa. Mwenyezi Mungu tunakuomba utufanyie wepesi kwenye zoezi hili. Amin
Rais Samia yupo Nchini Brazil kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi Wanachama wa Kundi la G20 mualiko wa Rais wa Brazil Mhe. Luiz Inácio Lula da Silva ambapo pamoja na mambo mengine, atashiriki mijadala inayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa na umaskini, kuchochea maendeleo endelevu na matumizi ya nishati mbadala.

RAIS Dkt. Samia Aongeza Muda wa Uokoaji Kariakoo
