MSUVA afikisha mabao 23 timu ya Taifa
MSUVA afikisha mabao 23 timu ya Taifa
Baada ya kufunga bao moja na kuisaidia Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia Katika mechi ya Kuwania Kufuzu Michuano ya AFCON 2025 Nchini Morocco, Simon Msuva amefikisha mabao 23 kwenye timu ya Taifa.
Katika Orodha ya wafungaji Bora wa muda wote katika kikosi Cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Msuva anashika nafasi ya pili nyuma ya Mrisho Khalfan Ngassa.
Orodha ya Wafungaji Bora wa Muda wote wa Taifa Stars.
- Mrisho Khalfan Ngassa – 25.
- Simon Happygod Msuva – 23.
- Mbwana Ally Samatta – 22
- John Raphael Bocco – 16.
Mabao hayo 23 ameyafunga katika michezo 93 tangu alipokitumikia kikosi hicho rasmi mwaka 2012, huku akibakisha mawili tu kuifikia rekodi ya Ngassa aliyefunga 25, kwenye mechi 100 alizochezea kuanzia mwaka 2006 hadi 2015.
Mbwana Samatta ndiye anayefuatia kwa ufungaji bora wa timu ya taifa baada ya kufunga mabao 22 katika michezo 82, tangu alipoanza kuichezea timu ya Taifa mwaka 2011, akifuatiwa na John Bocco mwenye mabao 16, katika michezo 84, aliyocheza kuanzia 2009.
Hata hivyo, rekodi zinaonyesha nyota anayeongoza kuichezea timu ya taifa michezo mingi ni beki, Erasto Edward Nyoni aliyecheza michezo 107 na kufunga mabao saba tangu alipokichezea kikosi hicho mwaka 2006 hadi 2021 akifuatiwa na Ngassa mwenye 100.
Nyota mwingine anayefuatia ni beki wa kati, Kelvin Yondani aliyecheza michezo 97, ya timu ya taifa bila ya kufunga bao kuanzia mwaka 2008 hadi 2021, akifuatiwa na Simon Msuva mwenye 93, huku John Bocco akiwa ameichezea timu hiyo mara 84.
Beki wa kulia Shomari Kapombe aliyeanza kuichezea timu hiyo kuanzia mwaka 2011, amecheza michezo 83 na kufunga bao moja akifuatiwa na Mbwana Samatta aliyecheza michezo 82, huku kipa, Juma Kaseja akicheza michezo 79, kuanzia mwaka 2002 hadi 2021.
Himid Mao aliyeanza kukichezea kikosi hicho kuanzia mwaka 2013, tayari ameichezea michezo 79 na kufunga mabao mawili tu huku kipa, Aishi Manula akifuatia kucheza michezo mingi baada ya kucheza 65, tangu alipoitwa mara ya kwanza mwaka 2015.
