Rais wa heshima klabu ya Simba SC, Bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’ ameeleza adhma yake ya kukamilisha uwanja na miundombinu mingine ndani ya Mo Simba Arena.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu ya Simba uliofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano Mwalimu Julius Nyerere leo tarehe 6,2024, Mo amesema kuwa ujenzi huo utakamilishwa baada ya mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji kumalizika.
Kwenye Mkutano huo, Mo aliweka hadharani ramani mpya ya ujenzi wa miundombinu inayotarajiwa kukamilishwa Mo Simba Arena akizitaka mamlaka husika kukamilisha mchakato wa ‘transformation’ ili mpango huo ukamilishwe.
MATANGAZO YA KAZI BOFYA HAPA
“Hii ni ramani mpya ya Mo Simba Arena Mradi mkubwa ambao utaweka msingi wa mafanikio yetu baadae”
“Tunatarajia kujenga kambi Bora ya mazoezi itakuwa na GYM, majengo ya malazi, kituo cha lishe, bwawa la kuogolea, kituo cha burudani, viwanja vitano vya kisasa zaidi ya hayo kujenga makumbusho ya klabu na kuanzisha chuo cha maendeleo ya vijana ili kulea vipaji vya soka nchini.”
“Ili kufanikisha yote haya tunasubiri mchakato wa mabadiliko ya Simba kukamilika. Tuko katika hatua za mwisho. Ujenzi wa miundombinu hii unakuja na gharama kubwa, ni ngumu kuanza huu ujenzi bila mfumo kubadilika.”
“Tukishirikiana tunaweza kujenga Simba inayoweza kushindana ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika, malengo haya sio ndoto, bali ni lengo linaloweza kufikiwa”
“Pamoja tunaijenga Simba ya kesho. Huu ni wakati wa kuchukua hatua kwa nguvu zaidi. Tukimaliza mchakato wa mabadiliko Simba itakuwa tayari kusimama imara na kujitegemea. Kwa heshima kubwa naomba tuache fitna, tuache fitna tuwe kitu kimoja. Tusigawanyike,” alisema Mo