MFUMO wa Serikali za Mitaa Tanzania
MFUMO WA SERIKALI ZA MITAA TANZANIA
Hii ni mada ya kwanza katika mfululizo wa mada za mafunzo ya awali kwa watumishi. Katika mada hii utajifunza maana, historia, sheria, uhalali, muundo, majukumu na mahusiano ya serikali za mitaa na serikali kuu katika kuchochea maendeleo kwa wananchi.
Malengo Mahsusi
Baada ya kujifunza mada hii utaweza:
|
1.2 Maana ya Serikali za Mitaa
Serikali za Mitaa hutafsiriwa kama vyombo vya wananchi ambavyo huundwa, huendeshwa, husimamiwa na kuwajibika kwa wananchi. Hapa nchini Tanzania vyombo hivi vimeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2 zinazobeba dhana ya ugatuzi wa madaraka. Yakupasa kuelewa kuwa Serikali za Mitaa ni sehemu ya serikali ambayo iko karibu zaidi na wananchi na inatoa huduma ambazo zinaendana na mahitaji ya wananchi husika katika eneo lao.
Angalizo
Tambua kuwa Serikali za Mitaa zinatokana na dhana ya ugatuaji wa madaraka kwa umma. |
Dhana na madhumuni ya madaraka kwa umma ni kuwapatia wananchi uwezo na fursa ya kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa, uchumi na uendeshaji wa nchi yao chini ya Ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba.
Swali la Tafakuri
Eleza dhana ya madaraka kwa umma katika undeshaji wa Serikali za Mitaa. |
1.3 Historia ya Serikali za Mitaa
Baada ya kujifunza maana ya Serikali za Mitaa, kipengele hiki kinakueleza kuwa Serikali za Mitaa zimepitia katika vipindi vitatu ambavyo ni kabla ya ukoloni, wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni.
1.3.1 Serikali za Mitaa Kabla ya Ukoloni
Mfumo wa Serikali za Mitaa umekuwepo tangu binadamu walipoanza kuishi pamoja ili kujilinda na wanyama au wavamizi. Kipindi hicho jamii ziliongozwa na watu waliokuwa wanaheshimika na wenye ushawishi. Baadhi ya jamii zilianzisha mabaraza ya wazee kwa ajili ya kujadili na kuamua masuala kuhusu usalama na ustawi wao. Kadiri jamii zilivyoendelea kukua, zilichagua machifu/watemi wa kuwaongoza wakisaidiana na mabaraza ya wazee.
1.3.2 Serikali za Mitaa Wakati wa Ukoloni
Katika kipindi hiki, nchi yetu ilitawaliwa na tawala mbili za kikoloni yaani Mjerumani na Muingereza. Kipindi cha utawala wa Mjerumani hapakuwa na juhudi mahsusi za kuanzisha Serikali za Mitaa kwani walitumia mfumo wa utawala wa moja kwa moja usioshirikisha wazawa.
Kipindi cha utawala wa Muingereza kulishuhudiwa juhudi za kuanzisha, kuendeleza na kudumisha mfumo wa Serikali za Mitaa. Sheria mbalimbali zilitungwa ikiwemo Sheria ya Mamlaka za Wazawa ya mwaka 1926 iliyowapa machifu mamlaka ya kiuongozi, kiutawala na kimahakama; Sheria ya Manispaa ya mwaka 1946 iliyoanzisha manispaa ya Dar es Salaam mwaka 1948; na Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1953 iliyoanzisha mfumo wa Serikali za Mitaa ambao kwa kiasi kikubwa ulirithiwa baada ya uhuru.
1.3.3 Serikali za Mitaa Baada ya Ukoloni
Serikali za Mitaa baada ya ukoloni zimepitia vipindi vikuu vinne ambavyo ni; miaka kumi ya kwanza ya uhuru, kipindi cha mfumo wa Madaraka Mikoani, urejeshwaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, na kipindi cha Maboresho ya Serikali za Mitaa.
Katika kipindi cha miaka kumi ya mwanzo wakati wa uhuru, serikali ya Tanganyika ilirithi sehemu kubwa ya mfumo wa Serikali za Mitaa wa utawala wa Muingereza lakini ilifuta Sheria ya Mamlaka za Wazawa ya mwaka 1926 ili kuimarisha umoja wa taifa changa la Tanganyika na kuanzisha rasmi Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mwaka 1972, serikali ilifuta Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuanzisha mfumo wa madaraka mikoani ambao ulilenga kupeleka mamlaka za serikali katika ngazi za msingi kuanzia ngazi ya Mkoa mpaka Vijiji. Mfumo huo ulishindwa kufikia adhma ya kuwashirikisha wananchi na kuboresha huduma kama ilivyotazamiwa.
Ni vema ufahamu kuwa kutokana na changamoto za mfumo wa Madaraka Mikoani ulioanzishwa katika aya iliyotangulia, serikali iliona umuhimu wa kurejesha mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 1982. Urejeshwaji huo ulienda sambamba na utungaji wa sheria mbalimbali za serikali za mitaa, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya Katiba ya nchi ya mwaka 1984 ili kutambua mfumo wa serikali za mitaa nchini. Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 zilitungwa ili kurejesha mfumo wa Serikali za Mitaa.
Baada ya kurejesha Mfumo wa Serikali za Mitaa, na kutokana na changamoto mbalimbali serikali iliamua kufanya maboresho ya serikali za Mitaa kupitia Sera ya Maboresho ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1998. Sera hiyo ililenga kuboresha maeneo manne yaliyojumuisha: Ugatuaji wa madaraka ya kisiasa, kifedha, kiutawala na maboresho ya mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, ili kuzipa Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM) uhuru na madaraka ya kutekeleza majukumu kwa ufanisi katika maeneo yao.
1.4 Sheria na Uhalali wa Serikali za Mitaa
Ni vema ukatambua kuwa, uhalali wa MSM unatokana na Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na unatokana na dhana ya kupeleka madaraka kwa umma. Hivyo, uundwaji, utendaji, maamuzi na uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa hufanyika kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria zilizotungwa na Bunge na miongozo mbalimbali. Rejea kielelezo Na. 1.1.
Kielelezo Na. 1.1: Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinazoelezea uhalali wa Serikali za Mitaa
Pamoja na Katiba ya nchi, pia, uendeshaji wa MSM huongozwa na sheria mbalimbali. Sheria hizi huainisha masuala anuwai kuhusu mfumo wa Serikali za Mitaa kama vile taratibu za uanzishaji, muundo na wajumbe, vyanzo vya fedha na namna ya kuendesha MSM. Sheria hizo ni pamoja na Sheria za Serikali za Mittaa (Mamlaka za Wilaya), Sheria za Serikali za Mittaa (Mamlaka za Miji), Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa (Utozaji) Kodi za Majengo, Sheria ya Serikali za Mitaa (Upendezeshaji) Majengo, n.k.
Angalizo
Ili kukujengea uwezo zaidi, soma Ibara ya 145 na Ibara 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sura ya 2. |
1.5 Muundo wa Serikali za Mitaa
Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 na Sheria za Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimegawanyika katika makundi mawili:
a) Mamlaka za Miji
b) Mamlaka za Wilaya
Mamlaka za Miji zinahusisha Halmashauri ya Jiji, Manispaa na Miji na Mamlaka za Wilaya zinahusisha Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Miji Midogo, na Halmashauri ya Kijiji. Tazama kielelezo Na. 1.2
Kielelezo Namba 1.2: Muundo wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
Ni vema ukatambua kwamba kimsingi Kata ni ngazi ya uratibu na siyo ya utawala, Hivyo ndivyo ilivyo pia kwa ngazi ya kitongoji kijijini na ngazi ya mtaa mjini. Ingawa viongozi (Wenyeviti wa Vitongoji na Mitaa) katika ngazi hizi huchaguliwa. Wao ni sehemu ya utawala katika ngazi ya kijiji au mji na wala siyo ngazi ya utawala inayojitegemea.
Chombo cha maamuzi katika ngazi ya Kata ni Kamati ya Maendeleo ya Kata. Mtendaji mkuu katika ngazi ya Kata ni Mtendaji wa Kata, ambaye ni Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Mtendaji wa Kata ni msimamizi wa watumishi na wataalam wote ngazi ya kata. Diwani wa Kata ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata. Jukumu kubwa la Kamati ya Maendeleo ya Kata ni kusimamia na kuratibu shughuli zote za maendeleo ya vijiji na mitaa.
Uendeshaji na Utekelezaji wa shughuli na majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ngazi zote, hufanyika kupitia utawala na utendaji ambapo viongozi wa kuchaguliwa kama wawakilishi na watendaji hushiriki pamoja katika kufanya maamuzi yanayowezesha ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, katika ngazi ya Halmashauri, baraza la madiwani ndicho chombo kikuu cha maamuzi ya Halmashauri.
Mtendaji mkuu wa Halmashauri ni Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ni msimamizi na mtendaji wa majukumu yote ya Halmashauri kupitia idara na vitengo. Idara na vitengo hivyo husimamiwa na wakuu wake ambao kwa pamoja huripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji. Kielelezo Na. 1.3 kinakuonesha muundo wa kiutendaji wa Halmashauri unaohusisha idara, vitengo na sehemu zote zinazowezesha utendaji kazi wa mamlaka husika kufanyika kwa ufanisi.
Kielelezo Na. 1.3: Muundo wa ndani wa Halmashauri
1.6 Majukumu ya Mamlaka za Serikali za Mitaa
Ni vema utambue kuwa shughuli na majukumu ya MSM yamegawanyika katika makundi yafuatayo:
Kutoa huduma za jamii
Kuweka mazingira mazuri ya kiuchumi
Kutekeleza programu za maendeleo
Kutoa huduma za ulinzi na usalaama
Kushirikisha wananchi katika kutoa maamuzi
Kusimamia matumizi ya fedha na uwajibikaji
- Kuweka wazi uendeshaji wa majukumu yao.
1.7 Mahusiano Kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa
Kwa mujibu wa Sera ya Maboresho ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1998 inaelekeza kwamba mahusiano baina ya Serikali za Mitaa na Serikali Kuu yatatawaliwa na sheria. Aidha mahusiano yatategemea mashauriano, majadiliano na maelewano badala ya kuegemea katika kutoa, kupokea na kutekeleza amri kama ilivyokuwa kabla ya maboresho ya serikali za mitaa. Kutokana na msimamo huo wa Sera, Sheria za Serikali za Mitaa Sura ya 287 na 288 (Vifungu 174 A na 54 A kwa mfuatano) zimeelekeza wazi jinsi mahusiano kati ya vyombo hivi yanavyopaswa kuwa, kwa kutaja majukumu ya Serikali Kuu, uwezo na kazi za Serikali za Mitaa.
Sheria za Serikali za Mitaa na Sheria nyingine za nchi zinaeleza kwa undani zaidi majukumu na mipaka ya Serikali za Mitaa na vyombo mbalimbali vya Serikali Kuu. Ili kuondoa mwingiliano huo mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa yanatawaliwa na sheria, na kamwe hayategemei maelewano kati ya viongozi na watumishi wa umma walio katika Serikali za Mitaa na Serikali Kuu.
Angalizo
Zingatia kwamba mamlaka za Serikali za Mitaa zina uhuru wa kutenda mambo yake bila kuingiliwa na serikali kuu. Uhuru huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria na unaweza kuingiliwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na sheria. |
1.8 Mahusiano Baina ya Watendaji wa Halmashauri na Viongozi wa Kuchaguliwa
Ni vema uhusiano baina ya watendaji na viongozi wa kuchaguliwa ukawekwa bayana. Viongozi wa kuchaguliwa katika mamlaka za serikali za Mitaa hujumuisha Madiwani wa Halmashauri, Wenyeviti wa Mtaa/Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji. Ili kujenga mazingira rafiki ya kiutendaji, viongozi na watendaji wanapaswa kuimarisha mahusiano baina yao.
1.8.1 Msingi wa Mahusiano Baina ya Madiwani na Watendaji
Sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 na 288 zilizaa Kanuni za Maadili ya Madiwani sawa na Tangazo la Serikali la mwaka 2000.
Kanuni ya 25 hadi 28 ya Kanuni za Maadili ya Madiwani, 2000 zinaeleza misingi itakayoongoza mahusiano kati ya madiwani na watendaji wa Halmashauri. Mfano, Kanuni ya 26 ya Kanuni za Maadili ya Madiwani, 2000 zinaeleza kuwa Madiwani na Watumishi wa Halmashauri watatakiwa kujenga uhusiano mzuri utakaohakikisha ufanisi na utendaji bora katika Halmashauri. Pia, hawana budi kuepuka uhusiano na watumishi unaoweza kuathiri au kudhalilisha upande mwingine
Katika kuboresha mahusiano Kanuni zinaelekeza kuwa: –
Diwani na mtumishi wawe na mahusiano mazuri wanapotekeleza kazi na shughuli za Halmashauri,
Diwani na watumishi wa Halmashauri waheshimiane
Kusiwepo na uhusiano wa karibu na mtumishi wa Halmashauri unaoweza kuathiri au kudhalilisha kila upande. Kwa mfano, mahusiano ya kimapenzi.
Diwani hapaswi kuingilia shughuli za kiutendaji za Halmashauri kama kushawishi au kushiriki katika tendo lolote litakalosababisha au kuchangia katika uongozi mbaya ndani ya Halmashauri.
v. Diwani ni mwakilishi wa wananchi, iwe ni kwa makusudi au uzembe anakatazwa kutoa taarifa za uongo au kutoa ushauri mbaya kwa Halmashauri.
1.8.2 Mahusiano Baina ya Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa na Watumishi
- Mahusiano bora baina ya Mwenyekiti wa Kijiji/Mtaa na watumishi ni chanzo cha ufanisi wa utekelezaji wa kazi na majukumu ya ngazi hizo.
- Hata hivyo mahusiano hayo yanapaswa kuzingatia mtiririko wa madaraka ya kiutendaji na utawala ndani ya Mtaa/Kijiji. Mtiririko wa madaraka unapaswa kuzingatia utaratibu kuwa masuala yote yanayohusu Mtaa /Kijiji yatawasilishwa na kuelekezwa kwa mtendaji wa kijiji/kijiji ambaye ni Mtendaji Mkuu wa shughuli zote za Serikali ndani ya Kijiji au Mtaa husika.
- Mwenyekiti wa Kijiji ni kiongozi Mkuu katika ngazi ya Kijiji na ndiye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kijiji.
Kisa Mkasa
Afisa Elimu Bwana Mwinyi ambaye pia ni mkuu wa Idara ya Elimu msingi aligomea maagizo ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chikuye yaliyomtaka kuwasilisha taarifa ya mahudhurio ya walimu wa shule ya msingi Ukuti iliyopo ndani ya kata ya Chipukizi. Akiongea kwa uchungu na masikitiko, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chikuye Mheshimiwa Timani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Chipukizi alitanabaisha kuwa, inawezekanaje kwa mtu tuliyemwajiri agomee kutekeleza maagizo niliyompa ya kuwasilisha taarifa kwangu na kujibu kwa kiburi eti mpaka aambiwe na Mkurugenzi na si mimi, licha ya kuwa nina taarifa kuwa kuna utoro uliokithiri kwa baadhi ya walimu katika shule hiyo, hali iliyosababisha kuwa na kiwango duni cha ufaulu na shule hiyo kushika nafasi ya mwisho ki wilaya na ki mkoa. Maswali: 1)Je, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ana uhalali wa kutoa maagizo kwa mkuu wa idara ya Elimu? 2)Je wewe kama mtumishi mpya una maoni gani kuhusu majibu ya afisa elimu msingi wa wilaya? 3)Kwa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizopo una ushauri gani kwa Halmashauri ya Chikuye? |
1.8.3 Madhara ya Kutokuwa na Mahusiano Mazuri Baina ya Viongozi wa Kuchaguliwa na Watendaji
Ndugu Mtumishi mpya, zipo athari nyingi zitokanazo na kukosekana kwa mahusiano mazuri baina ya watumishi na viongozi wa kuchaguliwa
- Halmashauri kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi
- Kukosekana kwa ufanisi na kushindwa kufanya vikao
- Wananchi kukosa imani na Serikali
- Kupoteza rasilimali mbalimbali ikiwemo muda, nguvu kazi, fedha n.k.
- Kukosekana kwa morali/hamasa ya kazi kwa watendaji
- Kusitishwa au kuvunjwa kwa Halmashauri.
Kielelezo Namba 1.4: Mahusiano Baina ya Viongozi na Watendaji (Chanzo: Tovuti ya Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, 3-5-2021)
