Abdihamid Moallon Mrithi wa Mousa Ndaw Yanga SC
Abdihamid Moallon Mrithi wa Mousa Ndaw Yanga SC
Klabu ya Young Africans rasmi imeachana na aliyekuwa kocha wao msaidizi raia wa Senegal, Mousa Ndaw.
Baada ya kuachana na Ndaw, muda wowote kuanzia sasa uongozi wa klabu hiyo utamtangaza aliyekuwa kocha Mkuu wa KMC FC, Abdihamid Moallon kuwa kocha wao msidaizi.
Aidha Yanga inaunda benchi jipya la ufundi kimyakimya ikiwa ni hesabu za kutaka kufanya mabadiliko kwenye eneo hilo, uamuzi ambao unaweza kumgusa mpaka kocha mkuu, Miguel Gamondi.
Licha ya Gamondi kurejea kazini Jana November 11-2024, tunazo taarifa kuwa Yanga wanataka kukamilisha taratibu za kupata makocha wapya kabla ya kutangaza uamuzi wa kuachana naye.
Kwa upande wa Klabu ya KMC FC, Meya wa Manispaa ya Kinondoni ambaye pia ndio mwenyekiti wa klabu wa Klabu hiyo, Songoro Mnyonge amesema kuwa amesikitishwa na kitendo cha klabu ya Yanga cha kumshawishi kocha wao mkuu Abdihamid Moallin ajiunge na Yanga bila wao kuwashirikisha.
Meya huyo amedai kuwa hata Moallin amewakosea sana, amejiuzulu bila kufuata taratibu na Yanga wamekosea zaidi na hawautakii mema mchezo wa mpira wa miguu sio tu ukiwa timu kubwa na una fedha unaamua kunyanyasa timu ndogo kitu ambacho sio sawa amedai Songoro.
Pia Songoro amesema kuwa hata ishu ya mtu mmoja kufadhili timu 5-8 zinazocheza Ligi moja sio sawa hata mamlaka zinazosimamia Mpira wa miguu hazitaki kuliona hilo ila ukweli ni kwamba anayetoa fedha ndio anayechagua nyimbo hili haliko sawa ndio maana mtu anajiona yupo sawa kufanya anachotaka.
